Parasa lepida
Mdudu
Viwavi wakiwa wadogo, hula tabaka la chini la majani. Mara nyingi uharibifu huanza kwenye ncha za majani ambako mayai hutagwa mwanzoni. Baadaye viwavi unahamia kwenye kingo za jani na hula sehemu kubwa ya sehemu hiyo ya majani. Kadri viwavi wanapokua, hatimae hula jani lote wakianza kwenye ncha na kubakiza sehemu ya katikati tu ya jani huku kukiwa na alama zinazoonekana. Kutokana na ulaji huo, mimea hushindwa kufanya usanidimwanga ipasavyo, na kusababisha mavuno kupungua. Ikiwa mimea iliyoshambuliwa na viwavi imeshatoa matunda, basi matunda hayo yanaweza kudondoka kabla ya kukomaa. Viwavi wanaweza kuonekana wakila kwa makundi. Kinyesi chao kinaweza kuonekana kwenye mimea.
Ili kudhibiti wadudu hawa bila kutumia kemikali, ni muhimu kuondoa viwavi kutoka kwenye mimea iliyoathirika. Kazi hii inapaswa kufanywa kwa kutumia koleo au kipande cha utepe, bila kuwagusa viwavi moja kwa moja. Mitego ya mwanga pia inaweza kutegwa ili kuwanasa na kuwakusanya nondo. Takribani mitego mitano ya mwanga inaweza kuwekwa kwa hekta ili kudhibiti wadudu kwa ufanisi.
Chagua dawa sahihi ya kuulia wadudu kutegemea na mahaitaji yako, ukifuata maelekezo kwenye lebo kwa uangalifu, na kuvaa mavazi ya kujikinga pamoja na glavu wakati wa kutumia dawa hizo. Pulizia dawa endapo tu uvamizi ni mkali.
Madhara husababishwa na Kiwavi Nondo wa Michirizi ya Bluu. Wadudu hawa hupatikana zaidi katika maeneo ya tropiki na wanaweza kuwepo mwaka mzima. Nondo huyu hupitia hatua kadhaa katika mzunguko wa maisha yao. Huanza kwa mayai ambayo hutagwa juu ya majani ya mimea. Baada ya kuanguliwa, viwavi wachanga huanza kula majani. Wakati wa ukuaji wao, viwavi hawa hubadilika ngozi zao mara kadhaa na kuwa na ngozi mpya. Hatimaye, huunda vifukofuko(mithili ya mfuko) vinavyowafunika (vinavyowalinda) na kupitia hatua ya pupa. Baada ya muda kupita, nondo kamili hutokeza kutoka kwenye vifuko na kuanza upya mzunguko wa maisha yao. Viwavi wa mdudu huyu wana miili ya kijani yenye mistari mitatu ya buluu hafifu na hukua hadi urefu wa sentimeta 3-4. Vifukofuko huonekana kama mbegu kubwa zenye gamba gumu mithili ya karatasi lililofunikwa kwenye hariri. Nondo majike na madume wana mpangilio wa rangi zinazofanana. Nondo hawa wana kichwa chenye rangi iliyo kati ya kijani na manjano, mwili wenye rangi nyekundu iliyochanganyika na kahawia, miguu yenye rangi iliyo kati ya kahawia na nyekundu, na kingo za kahawia kwenye sehemu za nje za mbawa.