Orthaga euadrusalis
Mdudu
Dalili zinazoonekana zaidi ziko kwenye majani. Lava hula majani machanga kwa kukwangua sehemu ya juu ya ngozi kati ya mishipa ya majani. Kisha hula majani haya kwa fujo, wakiacha mshipa wa kati na vishipa vidogo pekee. Hii husababisha makundi ya majani yaliyokauka, yenye nondo na yaliyonyauka. Unapotokea uvamizi mkubwa wa wadudu hawa, vitawi hukauka, na hivyo kuzorotesha mchakato wa usanidimwanga. Miti iliyoathirika inaonekana kutokuwa na afya na inaweza kutambulika kwa urahisi kutokana na majani yake yenye rangi ya kahawia, yaliyokauka, na yaliyojikusanya pamoja. Utengenezwaji wa vikonyo vya maua huathirika na hatimae kuathiri mchakato wa kuchanua maua na kuzaa matunda.
Tumia maadui wa asili wanaoshambulia vimelea wa nondo wa majani ya mwembe kama jamii ya nyigu wanaoitwa Brachymeria lasus, Hormius sp., na Pediobius brucicida, pamoja na wadudu wanaokula wadudu wengine kama vile Mbawakawa mkimbiaji na mdudu aina ya reduviid. Pulizia dawa aina ya Beauveria bassiana mara mbili au tatu wakati wa kipindi cha unyevu wa juu.
Daima zingatia mbinu jumuishi za usimamizi wa wadudu kwa kuchanganya hatua za kinga pamoja na matibabu ya kibaiolojia ikiwa yanapatikana. Inapendekezwa kupulizia mimea kwa dawa aina ya Quinalphos (0.05%) mara tatu kwa baina ya siku 15. Pulizia madawa ya kuua wadudu yanayotokana na lambda-cyhalothrin 5 EC( mililita 2 kwa lita moja ya maji), Chlorpyrifos (mililita 2 kwa lita moja ya maji), au Acephate (1.5 g kwa lita moja ya maji).
Uharibifu husababishwa na lava wa Orthaga euadrusalis. Majike ya nondo hutaga mayai yenye rangi ya kijani ya manjano iliyofifia kwenye majani ya mwembe, ambayo kwa kawaida huanguliwa ndani ya wiki moja. Kutegemea na hali ya hewa, kipindi cha lava kinaweza kutofautiana kati ya siku 15 hadi 30, kwa kuwa kwa kawaida kuna hatua tano za ukuaji wa lava. Baada ya hatua ya mwisho ya ukuaji, lava hubadilika na kuwa mabuu kwenye utando, huanguka chini kwa haraka, na kuendelea na mchakato wa ukuaji kwenye udongo. Kipindi cha kuwa mabuu kinaweza kutofautiana kati ya siku 5 hadi 15, kulingana na hali ya joto. Mashamba yenye miti iliyosongamana yana viwango vya juu vya uvamizi wa wadudu kulinganisha na yale ambayo miti imepandwa kwa nafasi na kuna usimamizi mzuri wa kanopi ya mti. Kwa kawaida uvamizi wa wadudu huanza mwezi wa Aprili na kuendelea hadi Desemba. Kiwango cha unyevu kina uhusiano mkubwa na ongezeko la idadi ya nondo wa majani.