Phyllocnistis citrella
Mdudu
Uvamizi wa wadudu unaweza kutokea katika hatua yoyote ya ukuaji na huwa unaonekana zaidi kwenye majani machanga. Dalili za awali zinaweza kuwa muonekano wa majani yaliyobadilika umbo, yaliyojisokota au yaliyojikunja, ambayo hata hivyo, hubaki na rangi ya kijani. Uchunguzi wa karibu unaonyesha njia nyeupe au za kijivu kati ya tabaka mbili za ngozi ya jani. Mchirizi mwembamba mweusi au mstari wa madoa meusi, unaolingana na kinyesi cha lava, unaonekana ndani ya njia/vihandaki hivyo, vinaonekana zaidi upande wa chini wa jani. Lava mara nyingi hupatikana mwishoni mwa njia hizo na lava kadhaa wanaweza kuwepo kwa kila jani moja. Uharibifu wa majani unaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya kuvu au bakteria. Uvamizi mkubwa unaweza pia kusababisha kupungua kwa kiwango cha usanisinuru, na kusababisha ukuaji uliodumaa, kupungua kwa ukubwa na ubora wa matunda. Katika hali mbaya, maambukizi ya chorachora wa michungwa yanaweza hata kusababisha kupukutika kwa majani yote ya mti na hatimaye kifo kwa miti michanga.
Wadudu wanaowinda ni pamoja na mbawakimia wa kijani wa jenasi/nasaba ya Neuroptora. Vilevile kuna aina mbalimbali za nyigu vidusia ambao hushambulia na kula lava wa mdudu chorachora/mchimba-jani la michungwa (yaani kanitangaze) miongoni mwa wengine, aina ya Tetrastichus. Viuatilifu vya kikaboni vinavyosheheni spinosad, sabuni ya utomvu wa mafuta ya samaki na mafuta ya Pongamia vinaweza kutumika kama dawa za kupulizia majani ili kudhibiti ushambuliaji wa kanitangaze wa michungwa. Mafuta ya mwarobaini pia yanaweza kutumika kuwazuia nondo wasiweze kutaga mayai yao kwenye majani.
Daima zingatia mbinu jumuishi na hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibayolojia. Dawa za kuua wadudu hazina ufanisi kabisa dhidi ya uvamizi wa kanitangaze wa michungwa kwa sababu lava wanalindwa na ngozi ya jani. Ikiwa dawa kuua wadudu zinahitajika, bidhaa za kimfumo na za kugusa zinapaswa kutumika wakati wadudu wakubwa wanapokuwa amilifu. Bidhaa kadhaa za madawa zinapatikana kama dawa za kunyunyizia, na miongoni mwa hizo ni zile zilizo na abamectin, tebufenozide, acetamiprid, diflubenzuron au spinetoram. Viuatilifu (dawa za kuua wadudu) vya familia ya pyrethroid ya viwandani pia vilitumika dhidi ya mdudu huyu.
Dalili zinasababishwa na shughuli za ulaji za lava wa chorachora wa jani la michungwa, anayefahamika kama Phyllocnistis citrella. Wadudu waliokomaa ni nondo wadogo sana, wenye rangi ya kahawia au kijivu wakiwa na mbawa zenye nyuzi nyingi na doa jeusi juu ya bawa la mbele. Wanakuwa amilifu zaidi (hai/wakishughulika) wakati wa hali ya ubaridi wa alfajiri na jioni, asubuhi mapema na usiku. Katika majira ya kuchipua, majike hutaga mayai yao upande wa chini wa majani. Lava wanapoanguliwa huwa na rangi angavu ya kijani au ya manjano na hula zaidi majani, ingawa matunda pia yanaweza kushambuliwa. Wanachimba vinjia/vihandaki kati ya tabaka mbili za ngozi ya jani, na kusababisha mashimo ya kijivu yenye mwonekano wa nyoka. Mwishoni mwa hatua ya lava, chorachora hutoka kwenye shimo na kuingia katika hatua yake ya pupa kwa kukunja jani kumzunguka. Ni mdudu hatari mkubwa wa mimea jamii ya machungwa, anayepatikana karibu katika maeneo yote makubwa yanayozalisha mazao jamii ya michungwa. Zaidi ya hayo, uwezekano wa kupata magonjwa mengine, kama vile bakteria wa vikwachu, huongezeka.