Agromyzidae
Mdudu
Mistari ya kijivu hafifu isiyo ya kawaida au yenye umbo mithili ya nyoka huonekana pande zote mbili za majani kadri lava wanavyokula. Mitaro hii kwa kawaida hukatizwa na vishipajani na ina vinyesi vyeusi vinavyoonekana kama alama nyembamba ndani ya vimtaro. Majani yote yanaweza kuwa na mashimo. Majani yaliyoharibika yanaweza kupukutika mapema kabla ya wakati (kupukutika kwa majani). Kupukutika kwa majani kunaweza kupunguza mavuno na ukubwa wa matunda na kuyaacha wazi kwenye jua kali. Ugonjwa huu usichanganywe na kidomozi wa nyanya (kanitangaze) ambaye mashimo yake kwenye majani ni mapana zaidi na yanakuwa na rangi nyeupe au angavu.
Nyunyizia bidhaa za mafuta ya mwarobaini (Azadirachtin) dhidi ya viwavi/lava kwenye majani asubuhi mapema au jioni. Kwa mfano, nyunyizia mafuta ya mwarobaini (15000 ppm) kwa kiwango cha 5ml/l. Hakikisha unafunika majani vizuri. Mafuta ya mwarobaini huingia kidogo kwenye majani na kufikia baadhi ya viwavi walioko ndani ya vihandaki. Matumizi ya nematodi entomophagous, Steinernema carpocapsae, kwenye majani yanaweza kupunguza idadi ya nzi kidomozi. Udhibiti mwingine wa kibiolojia wa nzi kidomozi ni pamoja na parasitoidi (kwa mfano Chrysonotomyia punctiventris na Ganaspidium hunteri) na nematodi (kwa mfano Steinernema carpocapsae).
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kinga pamoja na matibabu ya kibiolojia ikiwa yanapatikana. Dawa za kuua wadudu mbalimbali wakiwemo kutoka kwa familia za organofosfati, karbamate, na pyrethroids huzuia nzi wakubwa kutaga mayai, lakini haziui lava. Zaidi ya hayo, zinaweza kusababisha kupungua kwa maadui wa asili (wanaokula wadudu waharibifu) na kukuza usugu kwa vidomozi dhidi ya madawa ya kuua wadudu, ambayo katika mazingira mengine inaweza kusababisha ongezeko la idadi yao. Bidhaa za madawa kama vile abamectin, chlorantraniliprole, acetamiprid, spinetoram au spinosad zinaweza kutumiwa kwa mzunguko ili kuepuka vidomozi kuwa sugu dhidi ya madawa.
Dalili hizi husababishwa na nzi mbalimbali wa familia ya Agromyzidae, wakiwa na maelfu ya aina ulimwenguni kote. Wakati wa majira ya kuchipua, majike hutoboa tishu za majani na kutaga mayai yao, mara nyingi kando ya kingo za majani. Lava wanakula kati ya ubapa wa juu na wa chini wa jani. Lava hawa hutengeneza mitaro mikubwa myeupe iliyopinda pinda huku ikiwa na mabaki ya vinyesi vyeusi vilivyoachwa nyuma kadri wanapokula. Mara wanapokomaa, lava hufungua tundu kwenye sehemu ya chini ya jani na kuanguka chini, ambako wanapitia hatua ya kuwa buu. Mabaki ya mimea karibu na mimea inayohifadhi vijidudu vya magonjwa huwa ni sehemu mbadala kwa mabuu kukomaa. Vidomozi huvutiwa na rangi ya njano.