Xanthomonas citri pv. mangiferaeindicae
Bakteria
Dalili kuu za ugonjwa wa madoa meusi ya bakteria ya miembe huonekana kwenye majani na matunda, lakini vitawi vidogo na matawi pia yanaweza kuathirika ikiwa ugonjwa utakuwa mkali. Mwanzoni, vidonda vidogo vyeusi vyenye maji maji hujitokeza kwenye majani. Madoa haya huzungukwa na kingo za rangi ya njano na huzuia kuenea kwa mishipa ya majani. kadri ugonjwa unavyoendelea, madoa hukauka na majani yanaweza kudondoka, na hivyo kusababisha kupukutika kwa majani. Katika hatua za mwanzo, madoa mepesi yaliyolowana majimaji huonekana kwenye matunda yaliyoambukizwa. Baadaye, hubadilika kuwa mashimo yenye umbo la nyota, yenye rangi nyeusi, na yanayochuruzika utomvu wenye maambukizi ambao huvutia vimelea nyemelezi vinavyosababisha magonjwa mengine. Maambukizi madogo husababisha kupungua kwa ubora wa matunda, wakati matunda yaliyoathirika sana yanaweza kudondoka. Vidonda vinaweza kutokea na kusababisha matawi na mashina meusi yaliyopasuka, ambayo hatimae yanaweza kudhoofisha uimara wa mti.
Upuliziaji wa mara kwa mara wa dawa zenye copper oxychloride imethibitika kuwa na ufanisi katika kuzuia na kupunguza maambukizi. Wadudu wa kudhibiti kibaolojia kama Acinetobacter baumannii kwenye miti iliyoathirika pia wanaweza kupunguza bakteria hawa kwa ufanisi.
Daima zingatia matumizi ya mbinu jumuishi zenye hatua za kinga na matibabu ya kibaolojia ikiwa yanapatikana. Dawa za kupulizia zenye thiophanate-methyl au benzimidazole zinaweza kutumika kudhibiti ugonjwa huu.
Ugonjwa huu unasababishwa na aina ya bakteria aitwae Xanthomonas citri. Bakteria hawa wanaweza kuishi hadi miezi 8 ndani ya tishu hai. Bakteria huathiri miti kupitia vidonda na sehemu ambazo kiasili zinakuwa wazi. Vimelea vinavyosababisha ugonjwa huu vinaweza kuenea kutoka mti mmoja hadi mwingine au kati ya shamba na shamba kwa njia ya mvua inayopeperushwa na upepo au kupitia zana za kilimo zinazotumika katika shughuli za usimamizi wa shamba kama vile kupunguza matawi. Vinginevyo, kuenea kwa ugonjwa hutokea kupitia mbegu, miche, au vipandikizi au kwa kugusana hasa katika matunda. Joto linalofaa zaidi kwa maambukizi ya madoa meusi ya bakteria ni kati ya 25 na 30 °C. Unyevunyevu wa juu pia huchochea maambukizi. Vizuizi vya upepo au upandaji wa aina za miti yenye majani mengi kuzunguka shamba la miembe inaweza kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu.