Xanthomonas campestris pv. campestris
Bakteria
Mara nyingi, uharibifu kwenye majani ya kabichi huonekana tu mwishoni mwa majira ya joto. Dalili kuu hujidhihirisha kama mabaka ya manjano, yenye umbo la kabari (umbo l a V) kwenye ukingo wa majani, baadaye yakisonga kuelekea ndani kwenye jani na kuelekea chini kwenye shina. Dalili hii hutofautisha uozo mweusi na mnyauko Fusari, ambao dalili husogea kutoka usawa wa ardhi na kuelekea juu kwenye shina. Kadri ugonjwa unavyoendelea, sehemu ya jani yenye rangi ya manjano huongezeka ukubwa na kubadilika kuwa kahawia kadri tishu zinapokufa. Vishipajani hugeuka kuwa na rangi nyeusi katika hatua ya mwisho ya ugonjwa, na hivyo kupatikana jina lake. Hatimaye, jani huanguka. Vimelea vinaweza kuingia kwenye shina na kuenea kupitia mfumo wa mishipa, kitu ambacho huonekana kama pete ya rangi nyeusi inapokatwa karibu na uso wa udongo.
Kuogesha kwa maji ya moto kwa dakika 30 kwa joto la 50 °C ni matibabu yanayopendekezwa kwa ajili ya kusafisha mbegu. Njia hii haina ufanisi kwa 100% dhidi ya uozo mweusi lakini hupunguza kiwango cha ugonjwa kwa kiasi kikubwa. Changamoto ni kwamba inaweza kupunguza kiwango cha kuota kwa mbegu.
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kuzuia na matibabu yanayopatikana ya kibaolojia. Matibabu ya mbegu kwa maji ya moto yanafaa sana katika kuzuia uchafuzi wa mashamba. Matibabu ya majani kwa kutumia dawa za kuvu/ukungu zinazotokana na shaba kila baada ya siku saba hadi kumi yanaweza pia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa bahati mbaya, matibabu haya yanaweza kusababisha madoa meusi kutolea kwenye majani ya nje ya kabichi.
Dalili husababishwa na bakteria wanaonezwa na udongo, na wanafahamika kama Xanthomonas campestris, ambao huishi katika mabaki ya mazao yaliyoambukizwa au kwenye mbegu kwa hadi miaka 2, au kwenye magugu ya familia ya Brassica kwa muda mrefu zaidi. Ugonjwa huu unaathiri mboga nyingi za majani za familia ya kabichi (ikiwa ni pamoja na brokoli, kauliflawa, tanipu, figili, na kohlrabi). Bakteria husambaa kwenye mimea yenye afya kupitia matone ya maji na kuingia kwenye tishu kupitia njia mbalimbali, na miongoni mwa njia hizo ni majeraha ya mmea. Mara mimea inapokuwa imeambukizwa, ugonjwa huenea haraka kwenye kabichi zingine. Dalili za kwanza huonekana kwenye udongo na mbegu zilizochafuliwa kwenye kitalu cha kuzalishia mbegu. Hali ya mazingira inayofaa kwa bakteria hawa na mchakato wa maambukizi ni hali ya unyevunyevu wa juu na joto la 25 - 30 °C. Mazao yaliyopandwa kwa msongamano yanachochea hali muafaka kwa bakteria kuenea kwenye mimea jirani. Katika hali hizo, mavuno ya mazao yanaweza kupunguzwa kwa 75 - 90%.