Mahindi

Mkanda wa Jani na Baka la Ala ya Jani

Rhizoctonia solani

Kuvu

Kwa Ufupi

  • Mkanda wa mviringo na pete iliyobadilika rangi, vilivyotota maji hutokea kwenye majani na vifuko (ala za majani).
  • Kuvu walio mithili ya pamba ya rangi ya kahawia nyepesi hutokea kwenye tishu zilizoathirika.
  • Ugonjwa huenea hadi kwenye masuke/mbelewele.
  • Mimea yote inaweza kuwa na mabaka .

Inaweza pia kupatikana kwenye


Mahindi

Dalili

Ugonjwa hujitokeza kabla ya kipindi cha kuchanua kwenye mimea ya umri wa siku 40-50, lakini pia unaweza kutokea kwenye mimea michanga. Dalili hutokea kwenye majani, vifuko/ala na mashina na baadae zinaweza kuenea hadi kwenye masuke. Kwenye majani na ala za majani hutokea mikanda ya mviringo na pete kadhaa zilizobadilika rangi na kulowana, mara nyingi zikiwa na rangi ya kahawia, hudhurungi au ya kijivu. Kwa kawaida, dalili huonekana kwanza kwenye ala ya jani la kwanza na la pili juu ya ardhi. Kadri muda unavyoenda, ukuaji unaoonekana wazi wa vitu mithili ya pamba yenye rangi ya kahawia iliyofifia, ikiwa na vidoa vidogo, vya mviringo na vyenye rangi nyeusi hutokea kwenye tishu zilizoathirika na baadae vinaweza kuenea hadi kwenye masuke. Bunzi (gunzi) linalokua huharibika kabisa na kukauka mapema kabla ya muda wake huku maganda ya mahindi yakitoa nyufa. Ukali wa ugonjwa hutegemea na hatua ya ukuaji wa suke wakati wa maambukizi. Ikiwa miche inaathirika, sehemu zinazokua hufa na mimea yote inaweza kufunikwa kabisa na mabaka ndani ya juma moja.

Mapendekezo

Udhibiti wa Kiasili

Ili kupunguza matukio na ukali wa ugonjwa, mbegu za mahindi zinaweza kutakaswa kwa kuzizamisha kwa dakika 10 kwenye mchanganyiko wa 1% sodium hypochlorite na 5% pombe(ethanol) ili kuua vijidudu, kisha kuoshwa mara tatu kwa maji na kuzikausha. Matibabu ya ziada kwa kutumia mchanganyiko wenye Bacillus subtilis huboresha athari hii. Madawa yenye kuvu wanaofahamika kama Trichoderma harzianum au T. viridi pia zimetumika kwa mafanikio katika kupunguza kuenea kwa ugonjwa.

Udhibiti wa Kemikali

Daima zingatia mbinu jumuishi kwa kuchanganya hatua za kinga pamoja na tiba za kibaiolojia ikiwa zinapatikana. Mbegu za mahindi zinaweza kutibiwa kwa namna ya kuzipa kinga kwa kutumia dawa ya captan, thiram, au metalaxyl, kisha kuoshwa mara tatu kwa maji safi yaliyochujwa na kuzikausha kwa njia ya hewa. Dawa za kuvu za kupulizia zinaweza kuwa na tija kiuchumi wakati unapopanda aina ya mbegu zinazoweza kushambuliwa na hali ya hewa inasaidia ukali wa ugonjwa. Dawa zenye propiconazole zina ufanisi katika kuzuia dalili mbaya zaidi za ugonjwa.

Ni nini kilisababisha?

Dalili hizi husababishwa na kuvu wanaofahamika kama Rhizoctonia solani ambao huishi kwenye udongo, mabaki ya mazao yaliyoathirika, au magugu ya nyasi. Katika hali nzuri ya unyevu na joto (15 hadi 35°C, bora zaidi 30°C) mwanzoni mwa msimu wa upandaji, ukuaji wa kuvu huanza tena na kushambulia mimea mipya iliyopandwa. Katika unyevu anga wa 70%, maendeleo ya ugonjwa yanakuwa madogo sana au hayapo, lakini kwenye unyevu anga wa 90-100%, kiwango cha juu cha ugonjwa hujitokeza. Kuvu huenea kupitia maji ya umwagiliaji, mafuriko, na usafirishaji wa udongo uliochafuliwa na vimelea kupitia vifaa vya shambani au mavazi. Ugonjwa huu unapatikana zaidi katika hali ya hewa ya joto na unyevu anga katika maeneo ya tropiki na nusutropiki. Ni vigumu sana kuudhibiti kuvu hawa kwa dawa za kuua kuvu, na kwa hiyo, inahitajika kutumia mchanganyiko wa mbinu za usimamizi mara nyingi.


Hatua za Kuzuia

  • Tumia aina za mimea zinazostahimili ugonjwa huu, ikiwa zinapatikana.
  • Epuka upandaji wa mimea kwa wingi sana shambani.
  • Ondoa na choma mimea iliyoathirika baada ya mavuno.
  • Hakikisha shamba linakuwa safi na hujeruhi mimea.
  • Ondoa majani ya chini yaliyoathirika yanayogusa udongo pamoja na ala/vifuko vyake.
  • Mzunguko wa mazao unaweza kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa kwa kiwango fulani.

Pakua Plantix