Nyanya

Ukungu wa Majani ya Nyanya

Mycovellosiella fulva

Kuvu

Kwa Ufupi

  • Madoa ya kijani hafifu au manjano yaliyoenea kwenye upande wa juu wa jani.
  • Viraka vya rangi ya kijani ya zeituni hadi zambarau-kijivu upande wa chini.
  • Kukauka na kujikunja kwa majani.

Inaweza pia kupatikana kwenye

1 Mazao

Nyanya

Dalili

Dalili hutokea kwenye pande zote mbili za majani na wakati mwingine kwenye matunda. Majani ya zamani huambukizwa kwanza na kisha ugonjwa husonga polepole kuelekea kwenye majani machanga. Kwenye uso wa juu wa jani, madoa madogo, yaliyoenea, ya kijani hafifu au ya manjano yenye kingo zisizo dhahiri huonekana. Upande wa chini, viraka vya rangi ya zeituni hadi rangi ya zambarau-kijivu na laini hukua chini ya madoa ya jani. Hivi vinaundwa na miundo inayozalisha vijimbegu na wingi wa makundi ya vijimbegu (conidia). Baada ya muda, madoa yanapoongezeka, rangi ya jani lililoambukizwa hubadilika kutoka manjano (klorosis) hadi kahawia (nekrosis) na jani huanza kujikunja na kukauka. Majani huanguka kabla ya wakati, na kusababisha uharibifu katika hali mbaya. Mara chache, vimelea hivi husababisha ugonjwa kwenye maua au matunda ukiwa na dalili mbalimbali. Maua yanaweza kuwa meusi na yatakufa kabla ya matunda kuwekwa. Matunda ya kijani na yaliyoiva huwa na sehemu laini nyeusi isiyo na umbo maalumu kwenye mwisho wa shina. Kadri ugonjwa unapoendelea, eneo lililoambukizwa huzama, kavu na lenye mwonekano kama ngozi.

Mapendekezo

Udhibiti wa Kiasili

Matibabu ya mbegu kwa maji ya moto (dakika 25 kwa 122 °F au 50 °C) yanapendekezwa ili kuzuia vimelea kwenye mbegu. Kuvu Acremonium strictum, Dicyma pulvinata, Trichoderma harzianum au T. viride na Trichothecium roseum ni wapinzani wa M. fulva na wanaweza kutumika kupunguza kuenea kwake. Katika majaribio ya kwenye vitalu-nyumba ukuaji wa M. fulva kwenye nyanya ulizuiwa na A. strictum, Trichoderma viride strain 3 na T. roseum kwa 53%, 66% na 84% mtawalia. Katika sehemu ndogo, siki ya tufaa, vitunguu saumu au kunyunyiza maziwa na mchanganyiko wa siki inaweza kutumika kutibu ukungu.

Udhibiti wa Kemikali

Daima zingatia mbinu jumuishi na hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibayolojia ikiwa yanapatikana. Matibabu yanapaswa kufanywa kabla ya kuambukizwa wakati hali ya mazingira ni rafiki kwa maendeleo ya ugonjwa huo. Michanganyiko inayopendekezwa katika matumizi ya shambani ni michanganyiko ya klorothalonil, maneb, mancozeb na shaba. Kwenye vitalu-nyumba, difenoconazole, mandipropamid, cymoxanil, famoxadone na cyprodinil zinapendekezwa.

Ni nini kilisababisha?

Dalili husababishwa na kuvu Mycovellosiella fulva, ambae vijimbegu vyake vinaweza kuishi bila mwenyeji kwa muda wa miezi 6 hadi mwaka kwa joto la kawaida (vimelea visivyo mtegemea mwenyeji). Unyevu wa muda mrefu wa majani na unyevu zaidi ya 85% hupendelea kuota kwa vijimbegu. Joto lazima liwe kati ya 4° hadi 34 °C ili vijimbegu viweze kuota, na halijoto ya kutosha inayo fikia 24-26°C. Hali kavu na kutokuwepo kwa maji maji kwenye majani huharibu uotaji. Dalili kawaida huanza kuonekana siku 10 baada ya kuambukizwa na ukuaji wa madoa pande zote za jani. Kwa upande wa chini, idadi kubwa ya miundo inayozalisha vijimbegu huundwa na vijimbegu hivyo huenea kwa urahisi kutoka kwenye mmea hadi mmea kwa upepo na maji, lakini pia kwenye zana, nguo za wafanyakazi na wadudu. Kawaida kimelea huyu huambukiza majani kwa kupenya kupitia stomata wakati kuna kiwango cha juu cha unyevu.


Hatua za Kuzuia

  • Tumia mbegu zilizoidhinishwa, zisizo na magonjwa, panda aina sugu au zinazostahimili iwapo zinapatikana katika eneo lako.
  • Panda mapema ili kupunguza ukali wa ugonjwa.
  • Rekebisha nafasi kati ya mistari na kati ya mimea ili kuboresha mzunguko wa hewa na kupunguza unyevu kwenye taji.
  • Fuatilia kujua uwepo wa ugonjwa na ng`oa mimea ilishoathiriwa mara tu inapogunduliwa.
  • Epuka matumizi makubwa ya mbolea za naitrojeni.
  • Kukuza mzunguko wa hewa ndani ya kitalu-nyumba.
  • Hakikisha unyevu uko chini ya 85% na joto la usiku juu zaidi ya joto la nje (inafaa kwenye kitalu-nyumba).
  • Tumia umwagiliaji wa matone na epuka kumwagilia majani.
  • Tumia vigingi, nyuzi/kamba, au pogoa mmea ili kuuweka wima na kuongeza mtiririko wa hewa kuingia ndani na kuzunguka.
  • Ondoa na uharibu (choma) uchafu wote wa mimea baada ya mavuno.
  • Takasa kitalu-nyumba kati ya misimu na kudumisha viwango vya usafi wa kina wa zana na wafanyakazi.

Pakua Plantix