Cercospora beticola
Kuvu
Ugonjwa huu huanza kwenye majani ya zamani, ya chini kwanza na kisha kuendelea hadi kwenye majani machanga. Madoa yenye rangi ya kahawia isiyokolea au ya kijivu, huku yakiwa na umbo la mviringo au la yai (2-3 mm kwa kipenyo) huonekana kwenye majani na vikonyo. Tishu hizi zilizokufa zimezungukwa na ukingo wenye rangi nyekundu-kahawia. Madoa mara nyingi huungana, na katikati ya madoa hayo kunaweza kukauka na kutoboka, na kusababisha kutokea kwa matundu kwenye ubapa wa jani (athari ya tundu la risasi). Hatua kwa hatua majani pia hubadilika rangi, na kugeuka kuwa ya manjano kwanza na baadaye, kadri yanapokauka na kufa, hugeuka na kuwa na rangi ya kahawia. Ukiangalia kutokea mbali, mimea iliyoathiriwa inakuwa na mwonekano wa kuungua na inaweza kushikamana na kanopi. Madoa kwenye mashina na vikonyo hurefuka na mara nyingi huzama kidogo. Katika hali ya majani kulowana kwa vipindi virefu, kunaweza kutokea kuvu aina ya velvet wenye rangi ya kijivu iliyo na giza, hususani kwenye upande wa chini wa majani, na kwa usahihi zaidi chini ya madoa.
Tumia dawa za kibaiolojia za kupuliza kwenye majani ambazo hujumuisha madawa yanayotokana bakteria aina ya bakteria Pseudomonas fluorescens, Bacillus amyloliquefaciens, Bacillus subtilis na kuvu Trichoderma asperellum. Vinginevyo, matibabu ya maji ya moto yanaweza kutumika kusafisha mbegu dhidi ya kuvu na kuhakikisha afya zao. Madawa yanayotokana na shaba (kama vile copper oxychloride ) pia ni njia inayokubalika ya udhibiti katika kilimo-hai.
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibaiolojia ikiwa yanapatikana. Ili kudhibiti vimelea vya kuvu tumia dawa za kuua kuvu aina ya triazole (difenoconazol, propiconazole, cyproconazole, tetraconazole, epoxiconazole, flutriafol, nk), au benzimidazoles.
Ugonjwa huu husababishwa na kuvu aina ya Cercospora beticola, ambao huishi kwenye mabaki ya mimea kwenye uso wa udongo au kwenye tabaka la juu la udongo. Kuvu hawa vile vile wanaweza kuishi msimu wote wa baridi kwenye mimea mbadala inayoweza kuwahifadhi kama vile magugu (magugu ya nguruwe, mchicha pori, mbigili) ambayo yanaonekana kuwa chanzo cha maambukizi kwa viazi sukari. Hali muafaka inayochochea ukuaji wa Kuvu ni unyevu wa juu (95-100%), umande wa mara kwa mara na hali ya hewa ya joto. Matumizi makubwa ya mbolea ya naitrojeni huongeza athari za ugonjwa huo. Ugonjwa mara nyingi husambazwa shambani kwa hali isiyolingana, kwa kawaida huwa katika hali ya ukali zaidi kwenye maeneo yanayohifadhiwa ambayo yanaweza kusababisha kuwa na viwango vya juu vya unyevu. Kuvu hawa ni vimelea vya magonjwa ya majani ya viazi vitamu yenye uharibifu zaidi duniani kote. Maambukizi ya kuvu hawa hutofautishwa na magonjwa mengine ya majani (Alternaria, Phoma na madoa ya majani ya bakteria) kutokana na ukubwa mdogo wa madoa na uwepo wa alama nyeusi katikati ya vidonda.