Stagonosporopsis cucurbitacearum
Kuvu
Kwenye miche, madoa ya mviringo, yaliyolowana maji, yenye rangi nyeusi au kahawia hutokea kwenye majani ya mbegu na mashina. Kwa mimea ya zamani, madoa ya mviringo hadi yasiyo na umbo maaulumu, yakiwa na rangi ya kahawia iliyofifia hadi iliyokolea huonekana kwenye majani, mara nyingi kwenye kingo au karibu nazo. Madoa haya huongezeka ukubwa kwa haraka hadi jani lote linakuwa na mabaka. Vikwachu hutokea kwenye tishu za mishipa ya shina na ute unaonata wenye rangi ya kahawia kwa kawaida huzalishwa kwenye uso wa shina. Madoa meusi mara nyingi yanaonekana kwenye vidonda, yanayoashiria miili midogo ya uzalishaji wa kuvu (ukungu). Mashina yanaweza kuzungukwa na kitu mithili ya mkanda wa vikwachu na miche au mimea midogo inaweza kufa. Ikiwa maambukizi yanatokea kwenye mimea mikubwa, vidonda hukua polepole kwenye mashina karibu na kitovu/kiini cha uvimbe wa tishu. Mashina yenye vikwachu (vidonda) yanaweza kunyauka na kupasuka, kwa kawaida baada ya katikati ya msimu. Madoa madogo yaliyolowana maji hutokea kwenye matunda yaliyoathirika, huongezeka ukubwa hadi ukubwa usiojulikana, na kutokwa ute unaonata mithili ya gundi.
Kizudio (extract) cha Reynoutria sachalinensis inaweza kutumika katika mashamba yanayotumia kilimo hai. Mchanganyiko wa spishi ya Bacillus subtilis QST 713 pia umeonekana kuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa huu.
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibaiolojia ikiwa yanapatikana. Mchanganyiko ulio na dawa za kuua ukungu kwa kugusanisha kama kama vile chlorothalonil, mancozeb, maneb, thiophanate-methyl na tebuconazole ni mzuri dhidi ya ugonjwa huu.
Dalili za ugonjwa huu zinasababishwa na kuvu (ukungu) anayejulikana kitaalamnu kama Stagonosporopsis cucurbitacearum, ambae anaweza kuambukiza mazao kadhaa ya maboga kama vile matikitimaji, matango, maboga, maboga lishe, mumunya, n.k. Vimelea vinaweza kubebwa juu au ndani ya mbegu zilizoshambuliwa. Endapo hakuna mimea mwenyeji inayoweza kuhifadhi vimelea hivi, bado kuvu wanaweza kuishi msimu mzima wa baridi kwa hadi mwaka mmoja au zaidi kwenye mabaki ya mazao yaliyoathirika. Katika msimu wa kuchipua, wakati hali ni muafaka kwa ugonjwa huu, vijimbegu (viiniyoga) vya kuvu huzalishwa, na vijimbegu hivi huwa ndio chanzo kikuu cha maambukizi. Hali ya chepechepe, unyevu wa zaidi ya asilimia 85, mvua, na muda ambao majani yanakuwa yamelowana (kutoka saa 1 hadi 10) ni mambo muhimu katika kufanikisha maambukizi na utokeaji wa dalili. Joto bora kwa ugonjwa linatofautiana kutegemea na aina husika na linatofautiana kutoka takriban 24°C kwa matikiti maji na matango hadi takriban 18°C kwenye tikiti. Upenyaji wa vijimbegu ( viiniyoga) vya ukungu huenda unafanyika moja kwa moja kupitia epidemisi (yaani seli za gamba la nje katika mimea), na haihitaji kutokea kupitia stomata au majeraha. Kujeruhiwa, mashambulizi na mbawakawa wa matango wenye mistari, na ulaji wa vidukari (wadudu mafuta), pamoja na maambukizi ya ubwiri unga, hufanya mimea kuwa hatarini kwa maambukizi.