Puccinia hordei
Kuvu
Dalili za kwanza huonekana mwishoni mwa majira ya baridi hadi majira ya kuchipua, na zikionekana kama upele/malengelenge madogo, ya duara, yakiwa na rangi ya machungwa-kahawia yaliyozagaa bila mpangilio upande wa juu wa majani. Malengelenge haya yana vijimbegu vya kuvu ambavyo vitapandisha mchakato wa maambukizi kati ya mimea ya shayiri. Wakati mwingine malengelenge haya pia hujitokeza kwenye mashina, vifuko vya majani, na mashuke. Mara nyingi malengelenge huzungukwa na duara la mwangaza wa manjano au kijani. Baadaye katika msimu (mwishoni mwa majira ya kuchipua au mwanzoni mwa majira ya joto) malengelenge madogo meusi huanza kujitokeza polepole upande wa chini wa majani. Vifuko hivi vipya vina vijimbegu vya kuvu ambavyo baadaye vitaishi kwenye mashina ya mimea au mimea mbadala inayohifadhi vimelea ili kuanzisha upya mzunguko. Tofauti na malengelenge ya rangi ya kahawia, haya yenye rangi nyeusi hayaondoki unapo yapangusa kwa vidole.
Hadi sasa, hakuna suluhisho la udhibiti wa kibayolojia kwa kutu ya kahawia ya shayiri linalo patikana. Tafadhali wasiliana nasi ikiwa unafahamu kuna suluhisho lolote la kibayolojia.
Daima zingatia mbinu jumuishi yenye hatua za kinga na matibabu ya kibayolojia ikiwa yanapatikana. Kunyunyizia kwa wakati muafaka dawa kinga za kuua kuvu zinazotokana na prothioconazole kwa ujumla zitasaidia kudhibiti kutu ya kahawia. Pia kuna aina mbalimbali za dawa za kuua kuvu wa majani zinazopatikana kutibu kutu ya majani kwenye shayiri. Kwa uzuiaji bora, tumia dawa hizo wakati kutu ya majani inapogunduliwa mapema. Utumiaji wa ziada wa dawa unaweza kuhitajika wakati msimu ni muafaka kwa magonjwa ya kutu.
Dalili husababishwa na kuvu aina ya Puccinia hordei, mojawapo ya aina nne za fangasi ambao huchochea kutu katika shayiri. Viumbe hawa wanaweza kukua tu kwenye mimea ya kijani. Kwa upande wa P. hordei, huishi wakati wa majira ya joto kwenye machipukizi yaliyochelewa kuibuka na mimea mbadala inayohifadhi vimelea kama vile Nyota ya Bethlehem (Ornithogalum umbellatum). Halijoto ya joto (15° hadi 22°C) yenye unyevunyevu mwingi na mvua za mara kwa mara huchangia ukuaji wa ugonjwa, wakati siku zenye upepo mkavu husaidia kuenea kwa vijimbegu vya kuvu. Mashambulizi makali ya kutu ya kahawia katika shayiri hutokea hasa mwishoni mwa msimu, hususani ikiwa viwango vya juu vya naitrojeni vimetumiwa. Mazao yaliyopandwa mapema yanaambukizwa zaidi kuliko yale yaliyopandwa kwa kuchelewa, hususani wakati wa usiku unapokuwa bado ni joto. Hata hivyo, kutu ya kahawia kwenye shayiri sio tatizo sana ikiwa mazao yatatibiwa na dawa ya kuua ukungu.