Colletotrichum spp.
Kuvu
Sehemu zote za mmea zinaweza kuathiriwa na ugonjwa huu unaosababisha kuoza. Dalili zinazoonekana zaidi ni kuoza kwa matunda na tishu zilizobadilika rangi karibu na juu ya mizizi, pia huitwa kuoza taji. Wakati taji la mmea limeambukizwa, mmea wote unaweza kunyauka. Unaweza kuona ubadilikaji wa rangi kwa kukata wazi taji la mmea ulioambukizwa. Kuoza kwa matunda huanza kama madoa yenye rangi ya kawahia isiyokolea, yaliyolowana maji ambayo hutokea kwenye matunda yanayoiva, ambayo hubadilika na kuwa ya kahawia iliyokolea au nyeusi, majeraha magumu. Katika hali ya unyevunyevu, majimaji yenye rangi ya machungwa yanaweza kutoka kwenye majeraha ya matunda. Majeraha meusi kwenye vitumba na maua, na maua yaliyokauka ni dalili za mwanzo za maambukizi. Majani yanaweza pia kuwa na madoa meusi na kuharibika, lakini hali hii pekee haimaanishi kuwa mmea una chule.
Tafuta madawa ambayo yanabainisha wazi kwamba ni kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo. Dawa hizi zimetengenezwa kutoka kwenye bakteria au kuvu wenye manufaa. Dawa hizi hufanya kazi vizuri zaidi zinapotumiwa kabla ya ugonjwa kuanza. Hakikisha udongo wako unakuwa na afya kwa kudumisha na/au kuongeza mabaki ya viumbe hai na kuondoa mabaki ya mimea ya mwaka uliopita. Udongo wenye afya unaweza kuwa na viumbe vingi vyenye manufaa ambavyo huzuia vimelea vya magonjwa vinavyoenea kwa njia udongo.
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibaiolojia ikiwa yanapatikana. Ni muhimu sana kupulizia dawa wakati mimea iko kwenye hatua ya kutoa maua. Usisubiri hadi uone dalili kwenye matunda ndipo upulizie dawa. Tumia tu dawa za kuua kuvu ambazo zimeidhinishwa na serikali. Badilisha aina ya dawa ya kuua kuvu unayotumia ili kuzuia chule kuwa sugu dhidi ya dawa zenye ufanisi zaidi. Soma lebo ya dawa za kuua ukungu unazochagua na hakikisha kuwa umeelewa jinsi zinavyofanya kazi, na fuata maagizo na utaratibu wa kutumia dawa hizo. Baadhi ya lebo za dawa hizo zinaweza pia kusema kwamba zinaweza kutumika kwa mfumo wa matone katika awamu ya kupandikiza, ambayo inaweza kutoa ulinzi zaidi kwa mazao yako.
Chule ni ugonjwa wa kuvu/ukungu na ni moja ya magonjwa yenye uharibifu zaidi kwa stroberi. Unaweza kusababisha hasara kubwa katika msimu mzima wa ukuaji na baada ya mavuno. Ugonjwa huo kwa kawaida huingia shambani kwa kupitia upandikizaji mpya wa mimea ya stroberi. Vimelea vya ugonjwa vinaweza kuwepo lakini visionyeshe dalili zozote hadi halijoto na unyevunyevu uwe mzuri kwa ukuaji wa kuvu hawa. Ugonjwa hukua vizuri zaidi wakati kuna hali ya hewa ya joto na unyevu. Matone ya mvua yanapogonga ardhi, yanaweza kusukuma chembe za udongo hewani na kueneza ugonjwa huo. Hii hutokea zaidi ikiwa kuna upepo. Pia imeripotiwa kwamba vimelea hivyo vinaweza kuishi kwenye udongo na mabaki ya mimea kwa hadi miezi tisa na vinaweza kuambukiza magugu yanayoota karibu na shamba. Hata mwendo wa mashine na watu shambani unaweza kueneza ugonjwa huo.