Ramularia collo-cygni
Kuvu
Maambukizi ya kuvu/fangasi yanaweza kutokea mapema wakati wa ukuaji wa mmea lakini dalili za kwanza zinaonekana tu mwishoni mwa msimu. Katika hatua za mwanzo za ugonjwa, “madoa ya pilipili” ambayo ni madogo na ya kahawia yasiyo na mpangilio huonekana kwenye jani au ala. Baadaye, madoa haya hukua na kuwa na umbo la mstatili, rangi ya kahawia-nyekundu, yaliyokufa tishu na ukubwa wa milimita 1 hadi 3. Madoa haya yamezuiliwa na mishipa ya jani, yanaonekana pande zote za jani, na kwa kawaida huzungukwa na duara la mwanga wa kahawia iliyofifia au manjano. Katika hatua za baadaye za ugonjwa, madoa yanaweza kuungana na kutengeneza maeneo makubwa meusi na tishu kufa kwenye sehemu kubwa za jani. Dalili zinaonekana pia kwenye ala za majani na mashuke. Kwa kutumia kiookuzi (mithili ya lensi), makundi meupe ya ukuaji wa kuvu/ukungu yanaweza kuonekana upande wa chini wa majani. Uharibifu wa jani unaweza kusababisha kuoza mapema kwa majani na kupoteza mavuno.
Samahani, hatujui tiba mbadala dhidi ya Ramularia collo-cygni. Tafadhali wasiliana nasi ikiwa unajua chochote kinachoweza kusaidia kupambana na ugonjwa huu. Tunatarajia kusikia kutoka kwako.
Wakati wote zingatia mbinu jumuishi zinazotumia hatua za kinga pamoja na tiba za kibaiyolojia ikiwa zinapatikana. Dawa za kunyunyuzia majani za kuua kuvu zinazotokana na triazole zinaweza kutumika kama njia ya kuzuia na kama chaguo la tiba mara tu ugonjwa unapogunduliwa. Matibabu ya mbegu yanayopatikana kwa sasa hayana athari kubwa kwa kuvu.
Dalili husababishwa na kuvu/fangasi anayefahamika Ramularia collo-cygni ambae anaweza kuishi katika mbegu, mimea inayoota yenyewe, mimea mingine ya nafaka inayohifadhi magonjwa au mabaki ya mimea kwenye udongo. Vijimbegu husambazwa kupitia upepo na mvua. Ingawa maambukizi yanaweza kutokea katika hatua yoyote ya ukuaji wa mmea, dalili huonekana tu mwishoni mwa msimu, wakati wa mpito kuelekea ukuaji wa uzazi. Kuvu huingia ndani ya mmea kupitia matundu ya asili kwenye majani na hushambulia tishu za ndani, akitoa sumu inayodhuru mmea. Kuvu huhitaji unyevunyevu kwenye uso wa majani (unyenyevu wa majani baada ya mvua au umande) kwa ajili ya kuota na kukua. Hali ya hewa yenye unyevunyevu au siku za joto zilizo na umande huongeza ukuaji wa kuvu na kiwango cha maambukizi.