Puccinia sorghi
Kuvu
Madoa madogo huonekana pande zote mbili za majani na polepole huanza kuwa madoa madogo yenye rangi ya kahawia iliyofifia, na yaliyoinuka kidogo. Madoa haya ambayo kimsingi yanakuwa yamerefuka, baadaye hugeuka kuwa malengelenge yaliyo mithili ya unga na yenye rangi ya kahawia ya dhahabu huku yakiwa yamesambaa kama mabaka yaliyo pande za juu na chini za majani. Rangi inaweza kubadilika na kuwa nyeusi kadri mmea unapokomaa. Tofauti na magonjwa mengine ya kutu, kwa kawaida dalili hazionekani mara zote kwenye sehemu nyingine za mmea kama vile mashina, vifuko vya majani au maganda. Hata hivyo, mashina huwa dhaifu na laini na yanakuwa kwenye hatari ya kuvunjika au kuanguka. Tishu za majani machanga zinakuwa na uwezekano wa kuathirika zaidi na maambukizi ya kuvu kuliko majani yaliyokomaa. Mimea iliyoathirika katika hatua za awali inaweza kuonyesha ubadilikaji wa rangi na kuwa ya manjano kwenye majani na kufa, na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa mavuno ikiwa majani ya juu yataathirika.
Kwa sasa hakuna matibabu mbadala yaliyopo dhidi ya Kutu ya Kawaida ya Mahindi. Tafadhali wasiliana nasi ikiwa utapata taarifa yoyote inayoweza kusaidia kupambana na ugonjwa huu. Tunatarajia kusikia kutoka kwako.
Daima zingatia mbinu jumuishi zenye hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibaiolojia ikiwa yanapatikana. Matumizi ya dawa za kuua kuvu yanaweza kuwa na manufaa zinapotumika kwenye aina za mimea zinazoweza kuathirika. Pulizia majani mapema kwa dawa ya kuua kuvu/ukungu mwanzoni mwa msimu endapo inaonekana kutu itaenea kwa haraka kutokana na hali ya hewa. Aina kadhaa za dawa za kuua kuvu zinapatikana kwa ajili ya kudhibiti kutu. Dawa zenye mancozeb, pyraclostrobin, pyraclostrobin + metconazole, pyraclostrobin + fluxapyroxad, azoxystrobin + propiconazole, trifloxystrobin + prothioconazole zinaweza kutumika kudhibiti ugonjwa. Mfano wa matibabu unaweza kuwa: kupulizia mancozeb @ 2.5 g/l mara tu baada ya malengelenge kuonekana na kurudia kila baada ya siku 10 hadi kipindi cha kuchanua manua.
Ugonjwa huu husababishwa na kuvu Puccinia sorghi. Kuvu hawa hukaa msimu wote wa baridi kwenye mwenyeji mbadala inayoweza kuhifadhi vimelea vya kutu (aina ya mmea wa Oxalis) na hutoa vijimbegu/viiniyoga vya kuvu wakati wa majira ya kuchipua. Vijimbegu hivi vya kuvu vinaweza kusafirishwa umbali mrefu na upepo na mvua. Vijimbegu huanza mchakato wa maambukizi mara vinapotua kwenye majani. Maambukizi ya pili kutoka mmea mmoja hadi mwingine pia yanaweza kutokea kwa sababu ya upepo na mvua. Ukuaji wa ugonjwa huu huchochewa na hali ya unyevunyevu wa juu(karibu 100%), umande, mvua na joto la ubaridi kati ya 15 na 20°C (inaweza kutofautiana kutegemea na eneo). Hali ya hewa ya joto na ukavu hupunguza au kuzuia ukuaji wa kuvu/ukungu na matukio ya ugonjwa. Ugonjwa huu ni tatizo zaidi kwenye mimea iliyotumika kwa uzalishaji wa mbegu na mahindi matamu. Mimea inayolimwa kwa ajili ya chakula cha mifugo, bidhaa za viwandani, au usindikaji wa vyakula; mimea hiyo huwa haiathiriki. Mavuno hupungua kutokana na tija ndogo ya mimea na kuanguka kwa mimea.