Mycosphaerella sp.
Kuvu
Dalili za kwanza zinaweza kupatikana kwenye jani la 3 na la 4 lililofunguka kwa kuvu wote wa Sigatoka. Vidoa vidogo vidogo vya manjano hafifu (urefu wa mm 1-2) hutokea kwenye upande wa juu wa lamina (yaani sehemu bapa) ya jani, sambamba na vishipajani (Sigatoka ya Njano) na vidoa vya rangi nyekundu-kahawia upande wa chini (Sigatoka Nyeusi). Madoa haya baadaye hukua na kuwa madoa membamba, yenye rangi ya kahawia au kijani kibichi na umbo la mkono wa kisokotea nyuzi (spindle). Vidonda hivi hupanuka zaidi sambamba na vishipajani na kutengeneza michirizi myekundu yenye kutu yenye umbo la mstatili na iliyotota maji katikati na maduara ya mwanga wa njano (urefu wa milimita 4 hadi 12). Katikati ya michirizi hatua kwa hatua hugeuka rangi na kuwa ya kijivu ya kahawia hadi kahawia kamili, ikiwa ni ishara ya kufa kwa tishu. Kwenye kingo za majani, madoa huungana na kuunda vidonda vikubwa vinavyotokana na kufa tishu, vyenye rangi nyeusi au kahawia vilivyozungukwa na maduara (halo) yenye mwanga wa manjano. Kupasuka kwa majani hufanya yawe na mwonekano mbaya.
Udhibiti wa kibayolojia kwa kutumia dawa za kuua kuvu zinazotokana na Trichoderma atroviride una uwezo wa kuzuia ugonjwa na zinajaribiwa kwa ajili ya uwezekano wa kutumika kwenye mashamba. Dawa ya kunyunyiza ya Bordeaux inayotumiwa kwenye maeneo ya kupogoa inaweza kuzuia ueneaji wa ugonjwa kwenye sehemu hizi za mimea.
Daima zingatia mbinu jumuishi na hatua za kuzuia pamoja na matibabu ya kibayolojia ikiwa yanapatikana. Dawa za kuua kuvu zenye mancozeb, calixin au chlorothalonil zinaweza kutumika kama dawa ya kupuliza kwenye majani wakati ugonjwa haujaenea. Mzunguko wa dawa za kuua kuvu kama vile propiconazole, fenbuconazole au azoxystrobin pia hufanya kazi vizuri. Mzunguko huo ni muhimu ili kuzuia Kuvu kuwa sugu dhidi ya madawa.
Dalili za Sigatoka ya Njano na Nyeusi husababishwa na fangasi/kuvu anayeitwa Mycosphaerrela sp. na anatokea duniani kote. Ni moja ya magonjwa hatari zaidi ya migomba. Kuvu huishi katika tishu za mimea iliyokufa au iliyo hai, na hutoa vijimbegu ambavyo huenezwa na upepo au matone ya mvua yanayorusha udongo juu. Njia nyingine ya uenezaji wa magonjwa ni kwa usafirishaji wa mimea hai iliyoambukizwa, takataka za mimea au matunda yenye vimelea. Hutokea mara kwa mara katika maeneo yaliyo kwenye mwinuko wa juu na halijoto ya ubaridi, au wakati wa misimu ya mvua kwenye maeneo ya nusutropiki yenye mazingira ya joto na unyevunyevu mwingi. Joto muafaka kwa ukuaji wa Kuvu ni karibu 27°C na majani machanga ndio huathirika zaidi. Ugonjwa huo hupunguza tija ya mimea, ambayo hatimae huathiri ukubwa wa mkungu na kupunguza muda wa kuiva kwa matunda.