Embe

Ubwiri Unga wa Miembe

Oidium mangiferae

Kuvu

Kwa Ufupi

  • Mabaka meupe yenye poda ( unga unga) yanaonekana kwenye majani, maua, na matunda.
  • Kuharibika kwa umbo la majani na matunda kunatokea.

Inaweza pia kupatikana kwenye

1 Mazao

Embe

Dalili

Sehemu za mimea zilizoathirika huonesha mabaka madogo yanayotokana na ukuaji wa kuvu(ukungu) mweupe mithili ya unga unga. Katika hatua ya baadaye ya ugonjwa, ukungu (ubwiri unga) unaweza kufunika maeneo makubwa ya tishu. Majani na matunda ya zamani yanaweza kuonyesha rangi ya kahawia iliyochanganyika na zambarau. Majani machanga na maua yanaweza kufunikwa kabisa na vijimbegu (viiniyoga) vyeupe vya ukungu, kuwa ya kahawia na kukauka, hatimaye kufa. Pia majani yanaweza kuonyesha uharibikaji wa umbo halisi kama vile kujikunja kuelekea chini. Matunda yanaweza kufunikwa na unga mweupe, na katika hatua za mwanzo yanaweza kupasuka na kuonyesha tishu zilizo mithili magamba. Matunda yaliyoathirika hubaki yakiwa madogo, yaliyoharibika umbo, na hayawezi kufikia ukomavu.

Mapendekezo

Udhibiti wa Kiasili

Kupulizia dawa za kibaiolojia za kuua kuvu/ukungu, dawa ambazo zina bakeria wanaofahamika kama Bacillus licheniformis hupunguza maambukizi ya ubwiri unga. Vijidudu vya kuvu vinavyofahamika kama Ampelomyces quisqualis imethibitika kuwa na uwezo wa kudhibiti ukuaji wa ugonjwa huu. Matibabu ya mimea kwa kupulizia majani kwa dawa zinazotokana na salfa, asidi ya kikaboni, mafuta ya mwarobaini, koani, na asidi askobiki yanaweza kuzuia maambukizi makubwa. Zaidi ya hayo, maziwa ni dawa asilia ya kuua kuvu. Maziwa yanaweza kutumika yakiwa katika hali ya maji baada ya maziwa kuganda ili kudhibiti ugonjwa wa unga.

Udhibiti wa Kemikali

Daima zingatia mbinu jumuishi zinazohusisha kinga pamoja na tiba za kibaiolojia ikiwa zinapatikana. Dawa za kuua kuvu zenye chumvichumvi za monopotassium, hydrodesulfurized kerosene, aliphatic petroleum solvent, mancozeb, na myclobutanil zinaweza kutumika kutibu ugonjwa wa ubwiri unga miembe. Ili kupata matokeo bora, matibabu yanapaswa kuanza kabla ya utokaji wa maua au katika hatua za awali kabisa za utokaji wa maua. Matumizi ya mara kwa mara kila baada ya siku 7-14 yanapendekezwa ili kupata ufanisi mzuri.

Ni nini kilisababisha?

Vimelea vya ugonjwa wa ubwiri unga huishi kwenye majani ya zamani au kwenye machipukizi yaliyolala (bwete) kutoka msimu mmoja hadi mwingine. Ukitoa tishu changa za kwenye shina na mizizi, tishu zingine changa za sehemu zote za mti zipo kwenye uwezekano mkubwa wa kuathirika na kuvu. Pale ambapo hali muafaka imekidhi, vijimbegu (viiniyoga) vya kuvu (ukungu) hutolewa kutoka kwenye vimelea vilivyohifadhiwa chini ya majani au kwenye machipukizi na kusambaa kwenye miti mingine kwa njia ya upepo au mvua. Hali muafaka zinazochochea ugonjwa huu ni joto la mchana la kati ya 10-31°C na joto la chini la usiku, pamoja na unyevunyevu wa kati ya 60-90%.


Hatua za Kuzuia

  • Chagua aina za maembe zenye uvumilivu au zinazostahimili ugonjwa ikiwa zinapatikana.
  • Panda miti ya miembe kwenye maeneo makavu na yenye upitishaji mzuri wa hewa.
  • Punguza matawi na ondoa magugu marefu ili kupunguza uwezekano wa kutokea kuvu(ukungu).
  • Fanya kilimo mseto kwa kupanda pamoja mimea mingine isiyoathiriwa au kuhifadhi vijidudu vya ugonjwa huu.
  • Hakikisha kunakuwa na uwiano sahihi wa virutubisho vya udongo na epuka matumizi ya mbolea zenye kiwango kikubwa cha naitrojeni.
  • Ondoa sehemu za mimea zilizoathirika na haribu mabaki yoyote ya mimea.
  • Tibu mimea kwa kutumia mbolea zenye potasiamu fosfati.

Pakua Plantix